Radio Shahidi

Shahidi wa Amani

Papa Francisko ana laani mauaji ya kinyama nchini Somalia!

Like0 Dislike0

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 18 Oktoba 2017 ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana shambulio la kigaidi lililotokea hivi karibuni nchini Somalia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 300. Baba Mtakatifu ana laani kwa nguvu zote vitendo hivi vya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia, watu ambao wameteseka sana kutokana na vita pamoja na majanga asilia kwa miaka ya hivi karibuni. Baba Mtakatifu anasema, anasali kwa ajili ya kuwaombea watu wote waliofariki dunia kutokana na shambulizi hili pamoja na wale wote waliopata majeraha ili waweze kupona haraka na kuendelea na shughuli zao za kawaida! Baba Mtakatifu anasali kwa namna ya pekee kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Somalia na kumwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, kuwaongoa watu wanaopandikiza utamaduni wa kifo sanjari na kuwasaidia wale wote wanaojitaabisha kwa ajili ya ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Somalia!
Askofu Giorgio Bertin wa Jimbo Katoliki Djibouti na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Mogadishu anasema, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Somalia kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na hivyo kuondokana na utamaduni wa kifo unaopandikiza mbegu ya chuki na uhasama, mambo yanayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Juhudi hizi zinapaswa pia kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, ili haki, amani na maridhiano yaweze kurejea tena nchini Somalia.
Kanisa Katoliki limekuwepo nchini Somalia tangu mwaka 1904 na kuna umati mkubwa wa waamini waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Somalia. Hii ni changamoto kwa Waislam na Wakristo kuendeleza majadiliano ya kidini kwa kushikamana kwa ajili ya huduma kwa ndugu zao na kwamba, tofauti zao za kidini na kiimani kisiwe ni chanzo cha vita, machafuko wala mipasuko ya kijamii kwani wote wanaunda familia ya Mungu nchini Somalia.
Kuna watu wenye mapenzi mema, wanaoitakia Somalia mema, kumbe, hawa wanapaswa kuunganisha nguvu zao kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu, heshima, ustawi na mafao ya wananchi wa Somalia katika ujumla wao badala ya kuendekeza uchu wa mali na madaraka; mambo ambayo yameendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo kwa miaka mingi nchini Somalia. Wananchi wa Somalia wanaoishi ughaibuni wanaweza pia kuchangia kwa hali na mali, ili kuikwamua Somalia kutokana na machafuko ambayo yanaendelea kutesa watu wasiokuwa na hatia!
Wakati huo huo, Bwana Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani na kushutumu vikali mauaji yaliyotokea nchini Somalia, Jumamosi, tarehe 14 Oktoba 2017 na kusababisha watu zaidi ya 300 kufariki dunia kutokana na shambulizi la kigaidi na wengine 400 kujeruhiwa vibaya. Serikali ya Somalia inakishutumu kikundi cha kigaidi cha Al-Shabab kwa kuhusika na shambulizi hili.

Friday, October 20, 2017

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
CAPTCHA
This question is for testing whether or not you are a human visitor and to prevent automated spam submissions.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.
Back to Top